MJI WA DAR ES SALAAM.
Mji wa Dar es Salaam hapo awali ulijulikana kama MZIZIMA wala hapakupata kuwapo na habari zenye ukamilifu juu ya chanzo cha jina hilo, bali kuna mapokeo mbalimbali yenye kueleza tu chanzo chake.
Mathalani, yapo mapokeo yanayoelezea kuwa katika mwaka 1866 Sayid Majid (Mwarabu) Mtawala na mfanyabiashara tajiri toka Oman inasemakana uliujenga mji wa Dar es Salaam kwa kiasi Fulani na hasa Bandari ili kumrahisishia upakuaji na upakiaji wa bidhaa zake mbalimbali ziingiazo na zitokazo kwa njia ya baharini.
Kutokana na hali nzuri sana ya utulivu na usalama wa bandari walivyoiona wakati wakishughulikia mizigo yao, wakaamua kuita Bandari hiyo kuwa ni ya salama. Jina hili lilizoeleka mno hatimaye likawa ndio chanzo cha mji wote kuitwa Bandari ya salama na baadae ikawa Dar es Salaam kama ijulikanavyo hadi hivi sasa.
Mapokeo mengine juu ya jina Dar es Salaam ni kwamba, inasemakana kuwa walikuja Mzizima wahindi wawili wafanya biashara enzi hizo mmoja akiitwa Butu na mwingine Salama. Wahindi hao walijenga nyumba mbili kubwa, kila mmoja na yake. Nyumba hizo za biashara ziliitwa mabanda. Wakulima kutoka shamba walikuja Mzizima kuuza na kununua bidhaa mbalimbali kwa wahindi hao.
Katika hali isiyoeleweka wakulima hao walivutiwa mno kufanya biashara ya kuuza ama kununua kwenye banda la Salama kuliko Banda la Butu.
Hivyo basi wakulima hao walipokuwa wakikutana njiani walipoulizana kama walinunua ama kuuza wapi bidhaa zao, jibu mara nyingi lilikua Banda la Salama ama kama ilivyozoeleka hivi sasa Dar es Salaam. Kuna mapokeo mengine juu ya kupatikana kwa jina la Dar es Salaam kama ifuatavyo.
Inasemekana kuwa Wazungu walipotaka kuingia nchini Tanganyika (Tanzania) Waarabu ambao walitangulia kuja humu nchini kabla yao yalizuka mapigano makubwa kati yao hususan wajerumani na Waarabu, enzi hizo mtawala mzalendo alikuwa Mwinyimkuu Mshindo, mapigano hayo yalipofika mzizima ikapatikana suluhu kupitia mazungumzo, mapigano yakaisha. Hivyo sehemu hii ya mzizima ikapata jina la Bandari ya Salama kutokana na amani iliyopatikana wakati huo. Kwa hivyo jina la mzizima likabadilika badala yake pakaitwa
Banda la salama
Bandari salama
Bandari ya salama
Na hatimaye pakaitwa D’Salaam, Jina litumikalo hadi hivi sasa.
Wakati huo huo Bwana Hatimi Mfanya Biashara ya Chumvi Mwarabu alifika kwenye mwambao huo akaleta chumvi na akaoa mjakazi, binti wa Kishirazi na akabahatika kupata mtoto mmoja wa kiume.
Kwa kuwa Bw. Hatimi ndiye aliyeleta chumvi basi mtoto huyo akaitwa chomvi (chumvi) na baadae jina la chomvi likabadilika na kuwa shomvi, na kizazi chake kikaitwa Wamashomvi.
Inasemekana kuwa Wamashomvi ni mchanganyiko wa Waarabu na wenyeji wa pwani ya Dar es Salaam.
NB:
Kutokana na maelezo ya Bwana B.A. Kando ya juu ya upatikanaji wa chumvi bila shaka kuna tofauti ya ugunduzi wa chumvi na uchuuzi wa chumvi kama ilivyokuwa kwa Bwana Hatimi. Yeye hatimi alikua mchuuzi wa chumvi, lakini siye aliyegundua chumvi.
SULTAN SEYYID MAJID NA WAJERUMANI.
Sayyid majid hapo mwanzoni aliogopa sana utawala wa Pazi. Wazalendo aliowakuta akitokea kwao Oman Uarabuni.
Kwa sababu ya kutafuta mali kwa ajili ya maisha, Sultani majid alilazimika kuhamia Mzizima kunako Mwaka 1862 na Mwaka 1865 alianza kuujenga mji wa Dar es Salaam kwa kiasi Fulani.
Lakini, mnamo mwaka 1885 Wajerumani waliingia Mzizima na katika mwaka 1886 walianzisha utawala wao. Wajerumani waliweza kuitawala Tanganyika walipomtumia mtu wao mjanja mjerumani Karl Peters ambae mnamo 1885 alifanikiwa kufanya mikataba ya kitapeli kwa kuwahadaa Machifu wazalendo hapa nchini. Chifu Mangungu ni mmojawapo aliyetiliana mkataba na Karl Peters. Hatimaye kuanzisha dola yao mnamo mwaka 1885. Katika mwaka huo huo Wajerumani waliweka mpaka ya nchi Tanganyika ili waweze kuendesha dola yao bila hofu ya kuingiliwa na mataifa mageni mipaka hiyo inatambulika kimataifa hadi hivi sasa.
Mwaka 1893, Wajerumani wakiunganisha na msaada wa mfanyabiashara Mwarabu tajiri wa Bagamoyo Sheikh Sewa Bin Hadji walijenga Hospitali kubwa ya kulaza wagonjwa pale palipokuwa pakijulikana kama Malindi, eneo la Bandari ambalo karibu na kituo cha kati cha Polisi (Central Polisi Stn). Sewa Hadji alichangia Rupees 12,400 ambazo kwa wakati huo zilikuwa pesa nyingi sana.
Mwaka 1894 Wajerumani walianza kujenga Reli ya kati (Central line). Na katika mwaka 1914 Wajerumani walijenga soko la Kariakoo.
Lengo na madhumuni ya ujenzi huo hasa ilikuwa kuadhimisha kutawazwa kwa mfalme wao Kaiser Wilhem huko Ujerumani . Lengo hilo hata hivyo halikutimia, kwani mwaka huo huo vita kuu ya kwanza ya dunia ilianza na kuvuruga mpango mzima.
Vita hii huku kwetu ilikua kati ya Waingereza na Wajerumani na hata Wazalendo walihusishwa kwa namna moja ama nyingine. Waliposhindwa Wajerumani, Waingereza walichukua hatamu ya uongozi wananchi hii kunako mwaka 1921.
Jengo hilo la soko likatumika kama kambi ya Jeshi ya kuwekea vifaa vyao vya vita. Kwa Kiingereza waliita “Carrier Crops” Waswahili katika kukosea matamshi waliita” Kariakoo” Jina maarufu ambalo linatumika hadi hivi sasa.
Kama ilivyokuwa kwa Wajerumani, Waingereza nao walianza na Ujenzi wa shule ya Uhuru wavulana Mwaka 1921. Enzi hizo ilijulikana kama Kichwele Boys Middle School. Na mwaka 1935 wakajenga shule ya Uhuru Girls Middle School. Wakati huo ilijulikana kama Kichwele Girls Middle School. Na kunako Mwaka 1939 walijenga shule ya Mchikichini Primary School.
Mwaka 1949 ilianzishwa Kampuni ya usafiri Dar es Salaam iliyoitwa kwa kifupi DMT ama Dar es Salaam Motor Transport. Kampuni hiyo ilibadilishwa jina baada ya uhuru wa Tanganyika na kuwa shirika la usafiri la Taifa na kuligawa sehemu mbili (UDA/KAMATA).
UDA – Usafi Dar es Salaam na KAMATA – Kampuni ya Mabasi Tanzania ambapo Kampuni hiyo ya mabasi hayo yalibuniwa ili kusafiri mbali, Bara na nje ya Tanzania, kama vile Kenya Mombasa na Nairobi, Kampala Uganda, Ndola Zambia na kadhalika. Mpango huu ulianzishwa rasmi mnamo mwezi Julay 1969 uamuzi wa kuunda Kampuni hizi za usafiri Dar es Salaam na bara ulianza kutokana na ongezeko la haraka la idadi ya wakazi wa Dar es Salaam hasa, na ingawa nchi nzima ya Tanzania idadi ya watu ilikuwa ikiongezeka kwa kasi kila uchao lakini toka hapo mwanzo ilionekana kuwa Dar es Salaam ndio mji ambao watu wake wanaongezeka kwa kasi zaidi kuliko maeneo mengine ya nchi.
Mr. L. W. Swants, Mwandishi mmoja kati ya vile vitabu vinne alivyozungumzia mwandishi wa simulizi hii. Katika kitabu chake The Zaramo of Dar es Salaam, amesimulia jinsi ya kuongezeka kwa wakazi wa Dar es Salaam kuanzia Mwaka 1957. Bw. Swants ameainisha kuwa pamoja na wakazi wengine kufikia mwaka huo Wazaramo pekee walikuwa 33, 960 Dar es Salaam. Idadi hiyo ilikuwa ni asilimia 18.5% ya wakazi wote wa Dar es Salaam kwa wakati huo. Na baada ya hesabu za sensa katika mwaka huo idadi ya wakazi wote wa Dar es Salaam walikuwa 183,260.
MUHIMBILI HOSPITAL
Itakumbukwa kuwa , hapo nyuma kidogo kabla ya kujengwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili. Hospitali kubwa ambayo ilifananishwa na Muhimbili ni Sewa Hadji Hospitali. Hospitali hii ilijengwa wakati wa utawala wa Wajerumani kama tulivyokwisha eleza hapo nyuma.
Hospitali ya Sewa Hadji ilikuwa pale Malindi karibu na Central Polisi Station eneo ambalo hivi sasa linatumika na Bandari baada ya Jengo hilo kubomolewa kwa upanuzi wa Bandari hiyo.
Wajerumani vile vile katika Mwaka 1897 walilifungua rasmi jengo jingine la Hospitali ijulikanayo hadi hivi leo The Ocean Road European Hospital. Hospital ambayo kwa hivi sasa inatumika maalum kwa magonjwa ya Saratani.
Waingereza walipokaribia kutoa uhuru wa Tanganyika walijitahidi katika kujenga baadhi ya majengo kama vile walivyojenga majengo ya Hospital ya Muhimbili. Hapo zamani Muhimbili palikuwepo na mabanda madogo tu eneo la sasa ilipo University of Dar es Salaam Facult of Medicine ambayo yalikuwa yanajulikana kama Muhimbili Hospitali na matumizi yake ilikuwa utibabu hasa wa kina mama wazazi wajawazito na huduma nyinginezo ndogondogo.
Hapakuwa pakilazwa wagonjwa kama hivi sasa. Waingereza kwa hivyo wakajenga Hospital kubwa ya kulaza wagonjwa walipomaliza kuijenga Hospital hiyo kwa fedha zao Princess Magret mdogo wa Malkia Elizabeth II alikuja kufungua rasmi mnamo Mwaka 1957 alipokuwa ziarani Tanganyika. Jengo hilo likaitwa Princes Margreth Hospitali kwa heshima yake. Princess Magreth ameshafariki hivi sasa.
Jina la Sewa Hadji lilipendekezwa kuwepo pale Muhimbili kwa madhumuni ya kumuenzi mfadhili huyo.Kwani ilipobomolewa Hospitali ya Sewa Hajji kule karibu na kituo cha kati cha Polisi, enzi zile palijulikana kama Malindi hapakuwahi kuwepo jina la Sewa Hadji popote Tanganyika bila shaka wakubwa waliona haingekuwa ni uungwana kumsahau mtu aliyejitolea kuwahami wananchi wengi wa Tanganyika siku hizo bila ya kuwepo kumbukumbu yake ndipo jina lake likaingizwa katika mashujaa wetu. Na bila shaka Mashujaa wetu wazalendo Kibasila na Mwaisela habari zao zinaeleweka vyema katika Historia ya nchi yetu ya Tanzania.
UTAMADUNI WA WAZARAMO (LUGHA)
Bila shaka kila kabila duniani lina utamaduni wake na lugha yao ya asili ya mawasiliano. Wazaramo halikadhalika wanautamaduni wao na lugha yao ya asili ya mawasiliano. Lugha yao ya kizaramo ni maarufu na ni moja kati ya lugha za zamani sana katika jamii ya Watanzania . Wazaramo baadhi yao hasa wazee wale wa vijijini ni mahiri sana wa kuongea lugha yao hadi hivi sasa kinyume na wale wazaramo waishio mijini hususani Dar es Salaam. Wengi wao hawawezi kuongea lugha hiyo kwa ufasaha, napengine si ajabu kutoifahamu kabisa. Athari ambayo huenda imeanzia toka kuzaliwa kwao. Hii imetokana na wazee wenyewe kutowafundisha vizazi vyao, tokea udogoni. Kutokana na taathira hiyo basi lugha ya kizaramo imekuwa ikipoteza umaarufu wake kadri ya miaka inavyosonga mbele.
Lawama , hii kwa hivyo moja kwa moja inabebwa na wazee wenyewe kwa kutokuwa makini kwa kutoitilia lugha yao mkazo toka zamani katika kuiongea mara kwa mara ili na vijana wao wapate kuiga, kwa hivyo basi polepole lugha hiyo ikaanza kusahaulika hususan kwa wale waishio mijini hasa na hivyo basi hatimaye hata huko vijijini pia.
Pamoja na kwamba bado kuna baadhi ya Wazaramo ambao wanaongea lugha yao hiyo lakini hawaongei kwa ufasaha na wala si wazungumzaji wanaoipa umuhimu wa kutosha.
Kwa kuwa si Wazaramo wengi wanaoiongea lugha hii hivi sasa hata huko vijijini dalili za kutoweka kabisa ni dhahiri katika muda si mrefu sana ujao, iwapo kama hatua za dhati kuinusuru hazitachukuliwa haraka.
Kumbukumbu zetu zinaonesha kuwa lugha ya Kizaramo katika ukoo wetu wa Seseme, imeachwa kabisa kuzungumzwa toka wakati ule wa Mababu na Mabibi zetu kina mzee Hussein Hussein Seseme takriban sasa miaka mia na hamsini iliyopita hivi. Mzee Hussein na nduguze wawili mzee Omar na Mzee Abdalah hawakuwa na mazoea ya kuzungumza lugha ya kizaramo waziwazi badala yake waliipa kipa umbele lugha ya Kiswahili, lugha ambayo wameichukulia kama lugha yao mama. Hapakuwepo na mkazo kabisa katika kuzungumza kizaramo matokeo yake vizazi vyote katika ukoo huu wa Seseme hatuna taalum ya lugha hii.
Lakini janga hili la kutokomea kwa lugha ya kizaramo halikuanzishwa na ukoo wa Seseme tu bali ni kosa lililotendeka na jamii
NGOMA ZA HARUSI NA SHEREHE ZINGINEZO.
Inasemekana kuwa Wazaramo walikuwa na mkusanyiko mkubwa mno wa ngoma za asili hata yawezekana kuwa ni moja kati ya makabila yenye ngoma nyingi mno katika Tanzania ingawa nyingi sasa zimeanza kutoweka. Ngoma hizo hasa huchezwa nyakati za sherehe mbalimbali kama vile kwenye harusi unyago, mkole kwa mabinti wanawari, suna ama jando kwa wavulana ambapo mangariba hucheza ngoma ya msewe na sherehe zingine kadhalika katika kutekeleza kazi yao.
Ngoma za Wazaramo baadhi y ake zina mgawanyiko wa tofauti ya watu umri na jinsia. Vijana wadogo huwa na aina yao ya ngoma, watu wa makamo pia huwa na namna yao. Hali kadhalika wazee wake kwa waume kila mmoja huchezwa kivyake. Lakini kuna vile vile ngoma za mjumwiko wa jinsia zote na umri wowote, hizo ndizo nyingi mno na ndio hizo furaha za Wazaramo na ngoma zao hizo za asili Ngoma mathalani mkole na msondo ni ngoma zinazowahusu kina mama na kina dada vijana na kadhalika.
Ngoma hizo kwa kuzitaja majina yake ambazo nyingi mno ni, Mdundiko, Msondo, Vanga ama Mkinda, Mkwaju Ngoma, Matarumbeta ama Beni bati Mnanda ama Mchiriku, Mganda, Buti na kadhalika.
Na hapo siku za nyuma kidogo palikuwepo na ngoma ambazo hivi sasa husikika kwa nadra sana ama hazipo tena, kutokana na kupoteza kabisa umaarufu wake, ngoma ya Tokomile kwa mfano ilipoteza umaarufu wake kutokana na kufutwa kwa uhasama wa kijadi wa ngoma hiyo ambapo Mbango na Mizia mahasimu wakubwa walisababisha mapigano yasiyo na faida yoyote zaidi ya kumwaga damu bure tu kwa wananchi ambapo kinyume chake walikuwa wajenge umoja ili kuundoa ukoloni wa Mwingereza enzi zile kabla ya uhuru badala ya kuwa mbwa na chatu .
Mwalimu Nyerere wakati ule akiwa Mwenyekiti wa TANU chama kilichodai Uhuru wa nchi hii Tanganyika, rai yake kwa wananchi kuwa ngoma hiyo ichezwa bila ya silaha ili kuepusha mapigano na kumwaga damu kwa kuwataka Mbago na Mizia mahasimu hao wa jadi wapatane ili wawe kitu kimoja jambo ambalo lilionekana kama gumu sana hapo mwanzo lakini iliwezekana baadae uhasama ukamalizika na hatimaye ngoma yenyewe kufa kabisa. Siku hizi si rahisi kuisikia ngoma ya Takomile.
Kwa hakika ngoma ya Tokomile haikuwa ngoma ya amani, kama ilivyo desturi ya ngoma nyingi, kwani watu badala ya kufurahi walifanyiana uadui, ingawa Wazaramo wenyewe waliita ngoma ya mashujaa, hasa kutokana na yale mapigano baina ya pande mbili Mbango na Mizia lakini sababu hii haikuwa ya msingi hata kidogo.
Visa vingi viliwahi kutokea enzi hizo vya umwagaji wa damu na mara nyingine hata kusababisha vifo, kwa hivyo badala ya furaha ikawa ni misiba na vilio, jambo ambalo halikuwa na maana yoyote.
Ngoma ya Tokomile kwa makusudi kabisa wahusika walianzisha vurumai wakapigana ati kuonesha nani mbabe zaidi kati yao, hilo tu basi. Wala hapakuwepo na lolote la maana. Mwisho wa yote wakajikuta katika hasara kubwa. Ngoma zingine zilikufa kifo cha kawaida. Ngoma kama vile Ndalandala Mtondoo Lelemama Kasangwa, Ndekule. Sikinde na kadhalika. Ngoma hizo zilipata kuchezwa zama hizo za wazee wetu, Mababu na Mabibi, Vijana wa kizazi cha sasa si wengi walioweza kubahatika kuzishuhudia ngoma hizo zikirindima. Hivi sasa ngoma hizi imebakia hadithi tu kusimuliwa hamna la zaidi.
Kuna baadhi ya wanamuziki wa sasa wameziingiza baadhi ya ngoma hizo katika Bendi zao za dansi kama mtindo wao, kwa maana ya ubunifu katika kuboresha miziki yao .
Ngoma ya kina mama ya msondo kwa mfano. OTTU JAZZ imeungiza kama mtindo wao. Sikinde imeingizwa katika Band ya Mlimani Park na hata Ndekule iliwahi kuingizwa kwenye Safari Sound Band ya Huggo Kissima Mfanya biashara maarufu Dar es Salaam Band hiyo hivi sasa haipo tena. Hata hivyo uasilishaji huu wa mitindo ya ngoma hizo za Wazaramo katika miziki ya dansi hazikuweza kuzirudisha tena ulingoni bali ni kumbukumbu tu iliyobaki ngoma hizo kuwa zilikuwepo. Kulikuwepo pia vanga vanga Band ya Polisi Jazz zote hizo ni Ngoma za Kizaramo, ambazo Band za Music zilizitumia kama kitambulisho chao
NGOMA ZA MASHETANI NA TAMBIKO.
Ukiachana na ngoma za sherehe mbalimbali ambazo kwa kawaida ni za furaha, kuna ngoma zingine ni maalum kwa uganga. Ngoma hizo wateja hupunga mashetani, ni ngoma za tiba kwa wenye kupagawa na Pepo wabaya ama hupata maradhi yanayohusisha mashetani ambao inaaminika kuwa pepo hao huleta madhara kwa watu, kuumwa hata pengine kufa kama ukipambana na madudu hayo. Sasa , ili kumponya muathirika basi hupungwa mashetani kwa ngoma ya madogoli, pepo hao maarufu sana ni kinyamkera na mwanambago inaaminika kuwa ni lazima watolewe kutoka mwili wa mteja. Mteja ni Yule aliyepatwa na mashetani hao, hivyo mganga wa mashetani hulazimika kupigisha ngoma ya madogoli ili kumnusuru mgonjwa wake (Mteja)
Kwa upande mwingine kuna tambiko za jadi. Kwa kizazi hiki cha sasa, si rahisi sana kuelewa ama hata kukubaliana na mawazo ya wazee wa zamani hususani juu ya tambiko za jadi. Wazee wa zamani walisisitiza mno juu ya kufanya tambiko hizo za mizimu ya wahenga ambayo wanasema isipokumbukwa basi huenda ikaleta madhara makubwa kwenye ukoo mzima kama vile maradhi na hata vifo. Tambiko huwa kinga kwa husuda na kadhalika. Wazee waliamini hivyo.
Katika ukoo wa Seseme kwa mfano kuna tambiko la jadi linajulikana kwa jina la “GOMBO” Bado kuna kumbukumbu ya mzee mmoja mganga mahiri sana katika tambiko hii.
Akijulikana katika ukoo maarufu kwa jina la mzee “MCHAFU” Hata hivyo walikuwepo akina mzee Mchafu wengine wengi walioifahamu vyema “GOMBO” ala za ngoma hii ya Tambiko ni ungo wa kupetea nafaka, pamoja na udananda aina ya upinde mdogo ambao huwambwa kwenye ungo huo. na kisha mzee Mchafu ama mganga mwingine huvuta kamba ya upinde huo kama ilivyo namna ya udananda wa mwari wa kike afanyavyo ama mtu apigae gitaa upinde huo hutoa sauti ya kama mnyama Fulani aliyae kwa sauti ya chini chini ama sauti hiyo inaweza kufananishwa na gitaa la besi la Band hizi za sasa, lakini Gombo hutoa mlio mdogo zaidi wa chini chini.
Kwa hivyo washiriki wanaukoo wote hujumuika katika kucheza kwa kuzunguka zunguka wale wapigaji wa hiyo ngoma na kuimba kwa sauti kufuatisha maneno ya mganga aimbavyo.
Aghalabu nyimbo zenyewe hazipendezi masikioni mwa watu Tambiko hili huanza usiku kwani huwa za matusi makubwa bila kujali mjumuiko wenyewe umehusisha watu mnaostahiyana kiuzawa, kinachozingatiwa tu kwenye mkusanyiko huo ambao huwepo Baba, Mama, Babu, Bibi, Mjomba, Shangazi, Watoto, Wajukuu vilembwe na kadhalika ni ile miiko yao inayoruhusu kufanya hivyo ilimradi uganga utimie tu, wanavyoamini, hakuna tusi lolote litamkwalo litakalochukuliwa kama ni uvunjifu wa adabu, lau kama mtu atatukuna mbele ya mamaye ama babayake mzazi ama mzee yoyote ilimradi tu yupo katika tambiko hiyo basi yeye ni ruksa tu. Na hiyo ndiyo hasa maana ya “GOMBO”
Kwa hakika nachelea mno iwapo kamaTambiko la sampuli hii linawezekana kufanyika tena kwa uwepesi sana katika nyakati zetu hizi zenye nidhamu bora ya kidini, hususani dini yetu hii ya Kiislam, kama ilivyokuwa hapo zamani.
Kwa mujibu wa mafunzo ya dini ya Kiislamu ni kwamba Uislam haushirikishwi kwa vyovyote vile na mashetani, kwani mambo ya kishetani tayari yamelaaniwa kwenye Quraan Tukufu hivyo basi hayakubaliki Abadan.
Kwa asilimia kubwa sana Gombo linahusisha ushetani na si ajabu hata ushirikina pia umo. Hivyo tahadhari inalazimika sana.
Nyimbo ziimbwazo katika Gombo ni za matusi ya nguoni, lakini hakuna mwiko katika kuimba matusi hayo, hata kama utaimba mbele za watu mnaostahiliana kinasaba.
Gombolillaga x 2 kolila naumoyo Gombo kolilla naumoyo” x 2
Waganga huimbisha hivyo na wanandugu hulazimika kuitikia kwa kufuatisha maneno hayo kwa sauti kubwa ya kuhinikiza huku ngoma ya Gombo ikirindima.
Wengi katika sisi wanandugu, wajukuu wa akina mzee Makumbitu tukiwa tumechanganyika na wazee wetu, Baba zetu mama zetu shangazi zetu na kadhalika tumekuwa ni watu wa kufuata amri tu kutoka kwa wazee hao, lakini hatukupewa nafasi hata chembe kuhoji jambo lolote lile juu ya utamaduni huo wa Gombo, kwani kufanya hivyo ni kutaka kujua kile kinachoendlea katika tambiko hilo linalochukuliwa na wadau kama ni kuwakosea adabu wazee. Bila shaka jambo likishafikia hatua kama hiyo basi huwa halina sululu tena, bali ni kuacha tu amri ya wazee ichukue mkondo wake, na hivyo basi ndivyo ilivyokuwa.
Ngoma hii watu hukesha wakicheza na kuimba usiku kucha wakiwazunguuka zunguuka wale waganga walioketi katikakati yao, mithili ya mchezo wa kitoto wa Foriti.
Hakuna staili maalum ya uchezaji ngoma hiyo, ila wewe cheza tu vile uwezavyo na tamka matusi uyajuayo wala usiogope jambo lolote kwani hakuna mtu atakayekukosoa atakayesema kuwa wewe huna nidhamu. Kwani hivi ndivyo hasa Tambiko ya Gombo litakiwavyo. Tusi huwa si tusi katika Gombo bali huwa kinga kubwa dhidi ya maadui wetu kwa mujibu wa wazee wetu walivyoamini. Tambiko la ukoo wa Seseme”
Ifikapo Alfajiri wakati adhana inaposikika swala ya Kiislam huwa ndio kikomo cha Tambiko. Nyimbo za mwisho mwisho kumalizia shughuli nzima ya Tambiko, wanganga husikika wakiimbia:
“Sanze Mnumanunma, Sanze Mnumanuma, Kupitita bahano kadimanula manu, Sanze mnumanuma x 2”
Wimbo huo hurudiwa tena na tena, wanandugu hufikia na hatimaye mwimbo humalizika kuashiria kwisha kwa Tambiko.
Mganga Mkuu huamrisha wanandugu waliopo kwenye Gombo wakusanyike chini ya mti mkubwa ambao Gombo hufanyika, na kuamuru kila mtu kumega tonge moja la ugali uliopoa, ugali wenyewe huwa aidha wa ulezi au mtama lakini si wa mahindi. Pia kunyofaoa kipande cha nyama ya kuku wa kubanika wa dawa aliyepoa na kumeza mchangayiko bila kunywa maji wala kutafuna mfupa.
Kawaida miti iliyopendekezwa hasa kwa tambiko ni Mbuyu Mvule Mwembe na kadhalika.
Mifupa ya kuku, manyoya na utumbo hufukiwa pale chini ya mti pamoja na chungu kile kilichopikiwa ule ugali.
Wakati wa kuchimbia na kufukia chungu hicho cha dawa mganga mkuu huomba kwa niaba ya wanadungu mambo ya manusura katika Afya na kipato katika mwaka mzima husika maombi hayo hupitishwa kwenye mti ule.
Baada ya hapo mganga mkuu hutoa ruhusa ya wanandugu kurudi majumbani mwao hadi mwaka mwingine kwa ajili ya tambiko jingine.
Masharti ya Gombo ni kwamba nyimbo zile za Tambiko za Matusi ni lazima ziimbwe tena kwa sauti kubwa ili walio mbali waweze kusikia vyema nini kinachoimbwa.
Tena ziimbwe nyimbo hizo bila kuona haya wala kuweka staha kwa wazee mliojumuika nao, na bila ya kujali aina gani ya matusi yaimbwayo.
Wazee wetu waliamini ya kuwa gombo ni lazima katika ukoo huu wa Seseme, pamoja na kwamba hapakuwepo na maelezo yoyote ya kisayansi waliyoyaacha wazee hao juu ya umuhimu na ukweli hasa wa jambo hilo wanaloliamini kupita kiasi.
Jambo la ajabu kuhusu wazee wetu ni kwamba pamoja na wao huwa waumini wa dini ya Kiislam, dini ambayo inakemea vikali sana ushetani, lakini wao waling’ang’ania utamaduni wao huo walioachiwa na wazee wao, wa Tambiko la Gombo. Waliamini kuwa Gombo ni kinga kubwa sana katika ukoo.
Jambo hili kwa sasa linamvutano mkubwa sana baina ya Wazee na vijana, kuhusiana na Tambiko hilo la Gombo.
Sikuhizi Gombo hutekelezwa kwa shinikizo la wale wenye umri mkubwa kwa kuwapa maelekezo wadogo kama amri tu.
Lakini hapana shaka kuwa wakubwa hao katika ukoo nao ni waathirika wa mawazo ya wazee wao, Babu zetu. Kwa mantiki hii bila shaka Gombo sasa linaelekea kwenye hatima yake.
MARUHANI
Maruhani ni aina nyingine mojawapo ya mashetani, lakini husemekana kuwa ni mashetani wema kwa Binadamu. Kwani hufanya kazi ya tiba za maradhi mbalimbali badala ya kuwadhuru.
Wazee waliyatilia maanani sana Maruhani . Inasemekana kwamba yanaweza hata kuagua uchawi kwa mtu aliyerogwa.
Kwa kawaida huwepo waganga wanaotumia hawa maruhani katika ukoo.
Kwamba mtu aliyerogwa, shetani wa maruhani huwa na uwezo wa kugundua maradhi na mchawi aliyemroga mtu huyo.
Hivyo basi mganga wa maruahani huitwa kuja kumuagua mteja aliyerogwa .
Maruhani kwa jumla huwepo takribani katika kila ukoo hususan enzi hizo. Madhumuni hasa ya kuwepo hao maruhani ni kutibu inapotokea mtu kurogwa na kadhalika.
Hata hivyo kwa kusema hivyo sina maana ya kuwa Wazaramo walipendelea majini na uchawi la hasha bali hii ni kujulisha tu kwamba Wazaramo kama walivyo binadamu wengine wanafikwa na mambo mengi ya kidunia kama ilivyo kwa watu wengine wote hapa ulimwenguni.
UTANI KATIKA UZARAMO.
Kuna baadhi ya watu walikuwa wanawachanganya Wasukuma kama vile Wanyamwezi kwamba na wao pia ni watani wa wazaramo lakini kwa uhakika Wasukuma si watani wa Wazaramo ila tu kwa vile wasukuma na Wanyamwezi wanafanana mno katika mambo yao mengi hivyo basi moja kwa moja nao wamekuwa watani wa wazaramo.
Katika kutafiti ili kujua utani huo wa makabila haya ulianza vipi kwa kweli jibu lake halikupatikana bila shaka wazee wa zamani wanaweza kupata ukweli ulivyokuwa. Vile vile ndani ya Wazaramo wamo watani wanaotaniana wenyewe kwa wenyewe kwa mfano wanzala ni watani wa wavilindi na kadhalika.
Kuna utani pia kati ya Babu ama bibi na wajukuu zao. Utani kati ya mtoto wa mjomba na shangazi. Muhile kwa muhile na kadhalika.
Kwa mfano kuna utani wa mjukuu wa kiume na Babu na Bibi yake ulioandikwa na mtunzi mmoja BW. M. R. KIZARA katika kitabu chake UTANI wa TANZANIA (1975) Tunanukuu.
Mjukuu - Babu lelo nokwiza ikilo kuwasa na mtwanzi wako,
minyusile vinhugwe kwisha tena - “Zua diswa”
Babu: - Ikimbigalo kunacho mina cha kuwasa na
mtwanzi wangu.
Mjukuu: - Nielekelelo ulole
Babu: Segela hano govijo
Mjukuu: - Mbona koninga kodomba choni, nielekele ulole
Bibi: - Ikimbigalo kunacho avo cha kuwasa na nie?
Mjukuu: - Kama na bule mbona babu koninga kodumba msiwase
nangwe, leka aniluhusu ulole
Japo kuwa utani huu, unahisia kali sana, za ndani kihalisia, bado ulikua unakubalika katika jamii ya Kizaramo pasipo lawama zozote. Sina hakika sana kama hadi sasa utani kama huo unawezekana ukavumilika hata hivyo.
Bwana KIZARA ambaye amewahi kutembelea sehemu nyingi waanakoishi Wazaramo kama vile Msanga, Sungwi, Masaki na kadhalika, ametubainishia kuwa Wazaramo hawana watani wengi kama ilivyokuwa baadhi ya makabila mengine Tanzania
Bwana Kizara ameongeza kusema kuwa Wazaramo ni kabila tulivu mno ambalo halikupenda mapigano na jirani zao katika zama hizo na hata hivi sasa.
Ndugu wa Wazaramo hasa toka hapo asili ni Wakutu, Wadoe, Waluguru, Wakwele kwa vile wote hawa wanatokana na ukoo wa Pazi Kilama Lukali. Wazaramo toka enzi hizo walikuwa ni watu wapendao ushirikiano, urafiki, utani hasa kwa watani wao. Kwa jumla ni watu waliopendelea sana amani, hawakuwa wachokozi kwa hivyo hawakupenda kabisa vita kama ilivyo kwa baadhi ya makabila mengine Tanzania.
POSA ZA JADI ZA WAZARAMO.
Kwa kuwa tumepitia katika maeneo mengi mno kuhusu maisha ya Wazaramo na Tamaduni zao tumeona ni vyema pia tukaingiza jambo hili muhimu sana katika maisha ya binadamu duniani, jambo lenyewe si jingine bali ni “ndoa”.
Katika siku za nyuma kidogo mnamo Mwaka 1920 na kurudi nyuma masharti ya ndoa ya Kizaramo yafuatayo hapa chini ilikuwa ni lazima yafuaatwe iwapo wanandoa wawili inapofikia wakati wa kuhalalishwa kuoana vinginevyo ni vigumu mume kupata mke kwa namna yoyote ile, mambo yenyewe ni :-
Mahari
Mkaja
Kilemba
Behobeho
Kanyaga lubuga
Kisamula ndevu
Kilomo kinona
Mama Ngwaya
Kakulongela nani hano kama kuna Mtwanzi na kadhalika.
Baada ya Msululu wote huo kutimizwa ambayo tafsiri yake ni pesa ndipo ridhaa ya wazee kutolewa kwa binti yao kuolewa na muhusika.
Katika maandalizi muhimu ya harusi kuna ngoma mbalimbali ikiwemo mkole pia mwari kualikwa kuchezwa na kadhalika. Hapo mwari hufunzwa mengi kabla ya kuolewa lakini kama tulivyosema kuwa mambo hayo ni ya asili na yalitumika enzi hizo, lakini mengi kati ya hayo hivi sasa hayapo tena, na wala kizazi cha sasa hakina habari kabisa na utamaduni huu na kama yapo basi ni kitchenparty ambapo ni utamaduni wa kizungu hivyo mkole kwa sasa haumo katika mfumo wake wa zamani kwani mambo yameshageuka kabisa, badala yake ndio hiyo kitchen Party.