BW.ATHUMANI HUSSEIN HUSSEIN SESEME
je, unafahamu kuwa mzee Athumani ndio mtotot wa kwanza kati ya watoto 16 wa mzee seseme makumbitu?
fuatilia kwa makini historia yake.
Inakubalika kwamba safari yoyote ile haikosi kiongozi wake. Na katika uzawa wa ukoo huu wa Seseme hapana shaka kiongozi wake ni Bw ATHUMANI Hussein mtoto wa kwanza wa Mzee Hussein Hussein Seseme. Umefikiwa uwamuzi wa kumtambua hivyo mzee Athumani kuwa huyo ndiye kiongozi wa ukoo huo wa Seseme kutokana na yeye mwenyewe kufanya mambo mengi mazuri katika kusaidia ukoo kuimarika japokuwa mzee Athumani alikuwa mtoto wa tatu kiuzawa kuzaliwa. Baada ya kuanza kuzaliwa Bi Mwanakheri Omari Seseme, akifuatiwa na Bi Amina Abdallah Seseme ndipo kisha akazaliwa yeye bado fikra za wengi zilimpa nafasi kubwa ya uongozi Mzee Athumani. Ni mambo mengi mazuri alioyafanya katika ukoo huu ambayo yangefaa kupigiwa mfano lakini tunachelea kuandika hapa kila jambo kwani itakuwa ni hadithi ndefu kama vile alifu lela ulela. Kwa kifupi mzee Athumani alizaliwa mwaka 1922 bila shaka hapo Mtoni kwa Azizi Ally, na alifariki nyumbani kwake Bungoni Ilala Dar es salaam mnamo tarehe 29/9/2008.
ELIMU.
Mzee Athumani Hussein alipata elimu zote mbili ya dini na dunia , hivyo katika elimu ya dini ya Kiislamu imemjengea imani kubwa katika Uislamu hadi kuwa muumini wa kweli wa Kiislamu ambaye akifuata maagizo yote ya dini itikadi. Alikuwa Hamsa swalawat asiyependa kupitwa na hata kipindi kimoja cha swala katika umri wake wote hadi alipofariki.
Kwenye miaka ya hamsini hadi sitini alipata kuwa Imamu wa msikiti wa Keko Akida katika kipindi Fulani,, alipokuwa akiishi hapo kati ya mwaka 1952 hadi 1963 mzee Athumani alihamia Keko Akida katika mwka 1952 akitokea Mbagala, kabla ya hapo alipata kuishi mtaa wa Nyamwezi na Kipata eneo la Kariakoo mahala ambapo mtoto wake wa kwanza Bw. Hassan Athumani Seseme alipozaliwa kwenye miaka ya 1946 kabla ya kuhama tena na kurudi Mbagala kipindi chote hiki alishaanza kufanya kazi Railways alipoanza kazi Railwaya kunako mwaka 1940 akiwa na umri wa mika 19 hivi.
Akiwa kazini Railways alipata kupelekwa masomoni Nairobi Kenya katika kuboresha ujuzi wake kama Locomotive Mechanic katika idara ya fittingi shop. Na aliporudi masomoni akapata cheo cha foreman na hatimaye Supervisor. Cheo hiki alidumu nacho hadi pale alipostaafu rasmi mwaka 1977.
Alipohamia Ilala Bukoba Street 31 mwaka 1963 mwishoni aliendelea na Uimamu, hapo alisalisha msikiti wa Pangani na Mwanza mara baada ya kufariki Imamu wa msikiti huo kwenye miaka ya sabini themanini hivi.
Vile vile aliendelea na Uimamu katika msikiti mkuu wa Ilala, Arusha Street kwa muda fulani mwisho alimalizia uimamu katika msikiti wa masjid Taqwa Bungoni wakati huo alikuwa hajiwezi tena kwa kuzidiwa na umri na maradhi ya kiutu uzima.
Miaka ya 1977 alipostaafu kazi Railways alipata bahati ya kwenda HIJJAH MAKKA. Kutokana na kujishughulisha sana na mambo ya dini alipostaafu kazi alifanya kazi ya dini BAKWATA, kutokana na uadilifu aliwahi kuchaguliwa na BAKWATA kuwa Sheikh wa Wilaya ya Ilala cheo hicho alidumu nacho hadi kifo chake mnamo mwaka 2008.
Bwana Athumani katika elimu ya dunia alipata kusoma shule ya Mchikichini na hatimaye akaendelea na masomo yake katika shule ya Uhuru Mchanganyiko enzi hizo ikijulikana kama Kitchwele Boys Middle School. Hapa alisoma hadi darasa la nane kisha kujiunga na Railwaays 1940 . Kichwele Boys alipata kusoma na baadhi ya viongozi wa nchi hii Tanzania kama vile mzee Kawawa, Kitwana Kondo na kadhalika . Aliwahi pia kuwa kaka wa shule Prefect hapo Kichwele School.
Inasemekana kuwa elimu yake ya dini alisoma katika madrasa ya maalimu Mzinga eneo la Kariakoo lakini kwa vyovyote vile enzi hizo Masheikh waliokuwa wakifundisha walikuwa siyo hawa kina maalim Mzinga tunayemfahamu sisi. Kwani kipindi hicho tunachokiongelea ilikuwa miaka ya 1930/1940. Ni yule maalim Mzinga mwenyewe hapo awali aliwahi kusoma Madrasa ya baba yake Mzee Makumbitu hapo Mtoni.
Bw. Athumani aliwahi kuoa jumla ya wake wanne wakati wa uhai wake, kila mke kwa wakati wake, hakuwahi kuwa na mke japo wawili tu kwa wakati mmoja.
Mke wa kwanza wa mzee Athumani aliitwa Tuhuma bint Omari alimuoa mwaka 1940. Aliishi naye kwa takribani miaka mitano hivi, lakini Bibi huyu hakuzaa, alikuwa hana kizazi, mnamo mwaka 1945 alimuoa Bi Mwanaasha binti Mwinyihija Minjuma Kuchimba kutoka Mtoni Kijichi baada ya kumuacha Bi Tuhuma.Bi mwanaasha alizaliwa mwaka 1930 alipofunga ndoa alikuwa na umri wa miaka 16 tu.
Mzee Athumani alizaa watoto kumi na mbili (12) na Bi Mwanaasha mnamo mwaka 1969 Mzee Athumani alimwacha Bi mwanaasha na akaolewa na mume mwingine ambaye alizaa naye watoto wawili (2) Bi Mwanaasha baadaye aliugua na kufariki nyumbani kwao Mtoni Kijichi. Mnamo August 1981. Aliishi na mzee Athumani kwa miaka takribani 36 (1945- 1981)
Mwaka 1971 Mzee Athumani alimuoa Bi Meje kutoka Buyuni waliishi miaka ishirini na saba (27) alifariki, Bi Meje hakuwahi kuzaa na mzee Athumani. Mwaka 2000 Mzee Athumani alimuoa Bi Nyapilimo Akaishi naye miaka mitano kisha mnamo mwaka 2005 akamuacha. Baada ya hapo Mzee Athumani aliendelea kukaa bila ya mke hadi pale alipofariki 29/09/2008. Bi Nyapilimo alifariki mwanzoni mwa 2012.
1. Hussein athumani amezaliwa 1948 amefariki 1949
2. Chausiku Athumani amezaliwa 1950 amefariki 1952
Hadji Athumani amezaliwa 1956 amefariki 1997
Hadi sasa watoto walio hai ni saba (7) wakiwemo wanaume watano (5) na wanawake wawili (2) Watoto hao wanaume ni Hassan, Salama (Bapoo), Muharami, Omari na Ishaka wanawake ni Subira na Salima.
Mzee Athumani Hussein ni mmoja wapo kati ya mifano bora kwa binadamu kuiga kwani siyo siri yeye amefanya mengi mno katika uhai wake kwenye ukoo ambayo wengi wetu hatujayafikia mambo hayo. Mzee Athumani hakua mbaguzi katika ndugu zake na hata wasio kuwa ndugu zake.
Mzee Athumani tokea miaka ile ya 1950 wakati wazee wetu watatu wote wako hai akina mzee Hussein Hussein, Omari Hussein na Abdallah Hussein wameshampa fursa ya kuongoza ukoo.
Naye akakipokea cheo hicho kwa roho moja na kukitendea haki. Hii ni kutokana na tabia yake ya uadilifu.Dhamira ya mzee Athumani kwa ndugu zake ilikuwa ni kuwafikisha mbali kimaisha.
Na katika kuonesha jinsi alivyodhamiria kuwapeleka mbele kimaendeleo ndugu zake hao, wengi kati yetu alitulea kwa kutusomesha na kuhakikisha tunakuwa na maisha bora hapo baadaye,licha ya kuwalea wanawe wa kuzaa mwenyewe kama ilivyo wajibu lakini pia Bwana Jaffar Hussein Seseme, Mwishehe, Ashura, Ally na Husna ni kati ya wanandugu ukoo wa Seseme aliowahi kuwalea. Bwana Azizi Kuchimba, Bi Zena Kuchimba nao ni miongoni mwa hao aliowahi kuwalea. Hawa wakitokea upande wa mkewe. Pamoja na hao kuna wengine wengi aliopata kuwalea waliotokea aidha upande weke ama kwa mkewe, wote hawa aliwaona ni sawa hakujua kubagua.
Watu walimsifu kwa uungwana wake wamesema kuwa Mzee Athumani alikuwa ni muhimili mkubwa katika ukoo wa Seseme kwani hakujua kubagua yoyote wote kwake yeye walikuwa sawasawa mbele yake. Kwa kifupi cha maneno Mzee Athumani alifananishwa na Jemedari shupavu, Amiri, Khalifa na Imamu katika ukoo wa Seseme.
Bwana Athumani wakati wa mazishi yake pale Mbagala Kizuiani watu wengi mbalimbali walihudhuria, wakubwa kwa wadogo, wake kwa waume. Hiki kilikuwa kielelezo tosha cha umaarufu wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni